Friday, April 11, 2008

HOMA YA AKINA DADA KATIKA MAPENZI!!!

Mwanamke kumkubali mwanaume haraka ni dalili ya umalaya?

Namshukuru Mungu kunifanikisha hadi kuona jua la leo, na namshirikisha kila jambo nifanyalo. Karibuni tukumbushane machache juu ya mapenzi ambayo kila siku tumekuwa tukikumbana nayo, iwe asubuhi, mchana, jioni na usiku. Katika sekunde, dakika ama saa yeyote popote pale duniani.

Naweza kutafsiri mapenzi kama hisia nzito zimuingiazo mtu pale moyo wake unapozama katika ulimwengu wa huba kwa yule ampendae, akajikuta kwa lazima isiyoweza kuvumilika ama kukwepeka akampenda mwenzake.

Nadhani hakuna mtu asiyejua kupenda, ni wazi hata wewe unajua kupenda na ulishawahi kupenda na kupendwa, kama bado ipo siku mungu atakujaalia utampata umpendaye na akupendaye. Usikate tamaa mwombe mungu atakusaidi yeye ndiye anayejua mume gani au mke gani atakupa.

Na kama yupo asiyeweza kupenda basi huenda ana matatizo kisaikolojia na namshauri aende kwa wataamu wa mambo ya saikolojia waliopo karibu nae waweze kumshauri cha kufanya juu ya tatizo lake.

Wiki iliyopita nilizungumzia jinsi mtu anapojikuta akiwa mtumwa wa mapenzi kwa kulazimisha mapenzi kwa yule aliyempenda bila yeye kupendwa. Leo basi na penda kuongelea suala la mwanamke anapokuwa anatoa jibu la haraka kwa mtu anayemtongoza.

Kwanza unapomtongoza mwenzako unategemea kupata majibu mawili, eidha kukubaliwa ama kukataliwa. Na unapotongozwa unatarajia kutoa jibu moja la uhakika lisilo na kejeli, kumkubali ama kumkataa. Hii itategemeana kiasi mwanaume huyo atakavyo kukonga moyo wako na kukufanya uwe na msisimko wa kumtamkia hisia zako. Tatizo linakuja pale mwanaume anaposhituka na kuhofu kukubaliwa kwa muda mfupi na mwanamke aliyemweleza ukweli kutoka moyoni mwake.

Mpe wenzio uhuru wa kusema, mbona wewe ulimweleza bila kujali ni muda gani umekutana naye?. Kwanini tusibadilike, tukaenda na wakati?. Lazima tujiulize kulikoni inafikia hatua ya kumfikiria mtu uliyemtamkia anapokutamkia ukamuhukumu bila kosa.

Naomba ufahamu kitu kimoja, sisi wote ni binadamu, mwanaume anavyo penda hata mwanamke naye ana hulka ya kupenda na kumwonyeshe mwenza wake kiasi alivyo mpenda.

Pengine katika mila na desturi za sisi waafrika tulizoeshwa kwamba mwanaume ndiye mwenye kumrubuni mwanamke hadi kuwa naye katika ndoa, Inapofikia hatua ya mwanamke kutoa maamuzi itategemeana na mtu aliyemrubuni.

Lakini sidhani kwamba kuna ubaya mwanamke unapomtongoza ukategemea kupata jibu baada ya mwaka au mwiezi sita baadaye.

Kufanya hivyo si ishara kwamba huyo unayetegemea kupata jibu kwake atakuwa mwanamke mwaminifu sana, na atakuwa na tabia nzuri kupita yule atakaye kukubalia siku chache baada ya kumweleza bayana kile kilicho moyoni mwako.

Mwanamke ana haki ya kutoa msisimko wake juu ya yule aliyemtamkia ikiwa moyo wake nao umeridhia na kupendezwa na mwanaume aliyemtamkia kwa uwazi kwamba anampenda. lAkini hata hivyo nawashauri, kuwa makini sana na majibu ya watu wanau watamkia kuwa wanawapenda, usidanganyike na mali ya mtu ama cheo cha mtu, utakuwa unajiangamiza. Angalia utu na upendo wa mtu, usitizame pesa ambazo hata wewe waweza kuzipata, kumbuka pesa inaisha lakini utu wa mtu hauishi.

Kutamkiwa haraka na mwenzio uliyempenda si tiketi ya kumdhania mwanamke yule ni mdhaifu na malaya, wengine kuhofia huenda akawa akimkubali kila mwanaume atakaye mweleza anampenda. Naweza kukuhakikishia wanawake wengi hivi sasa wanajaribu kuwa wagumu kuwakubalia wanaume wanauwapenda kwa dhati kwa sababu wanaume wengi wamekuwa na hulka ya kizamani. Kama ulikuwa hutaki jibu mapema basi usingemtamkia mwenzako kwamba unampenda na una subiri jibu kutoka kwake.

Darubini yangu ya mitaani inaonyesha wanawake wengine wanajifanya wagumu kuwakubalia wanaume ilhali wanawapenda, kwa kuogopa kutoswa. Inapofikia hatua ya kuwazungusha wenzao muda mrefu waliowapenda wakajikuta kupoteza bahati zao. Kwani wanaume wengine wamekuwa wakiudhiwa na tabia ya wanawake wanaojifanya wagumu kama reli kumbe si waaminifu hata kidogo lengo lao waonekane wagumu kushawishika kwa wanaume wengine. Unaweza kumkuta mwanaume anatamba wazi wazi bila aibu, “Mimi namwamini sana demu wangu, alinizungusha mwaka mzima bwana. Inaonekana ni mwaminifu sana” Hicho sio kipimo cha uaminifu katika mapenzi, ndugu yangu. Tena anaweza akawa mgumu kwako pengine uchochoro kwa wengine.

Jaribu kuupa moyo wako uhuru, uchangue upendavyo, Usiudhulumu nafsi yako kwa sababu zisizo na msingi, kama unataka kumchunguza tabia zake ni jambo ambalo utafanya siri kabla ya kufikia hatua lengwa. Ukiubania moyo wake nisawa na kulinyima tumbo chakula, utateseka na hata amani ya moyo itatoweka. Usiunyime moyo wako uhuru.

NB: Ushauri wangu; Tunapaswa kubadilika, mwanamke anapomtamkia mwanaume aliyemtongoza kwa haraka si tiketi ya umalaya. Tuwe waaminifu katika ndoa zetu, uchumba na urafiki wetu, tusiwaudhi wandani wetu na kuwalaumu pasina sababu. Kufanya hivyo nikupunguza upendo wa dhati.

No comments: